Ndugu Wananchi,
Leo ni siku ya Mashujaa. Siku hii kila mwaka tunawakumbuka mashujaa wetu waliojitoa kupigana na wavamizi kutoka katika nchi za nje au wageni waliotaka kuitawala nchi yetu. Tunawakumbuka, kwa heshima, wale walio-pigana kuwazuia Wakoloni wasiitawale Tanzania, na waie waliopigana katika vita vya Maji Maji katika jitihada za kupinga utawala wa Kijerumani.
Wachache wao tuna-wafahamu, na majina yao tunayaheshimu: mashujaa kama Mkwawa, Mirambo, na Mputa. Lakini wengi wao hatuwafahamu kwa majina; ila tunafahamu tu ya kwamba waiipigana, na kufa, katika jitihada za kutetea uhuru wa nchi yetu. Tunawakumbuka na kuwaheshimu.
Leo tena tunawakumbuka mashujaa hao kwa fahari. Juhudi zao na vitendo vyao vilitutia moyo siku za nyuma na vinatutia moyo mpaka sasa. Hatutawasahau.