Ujamaa ni Imani

Ujamaa ni Imani, Hotuba aliyoitoa Mwalimu Julius K. Nyerere, tarehe 2, Novemba, 1978

Nimewaombeni tukusanyike tena hapa niwaelezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua, lakini nadhani si vibaya nikilieleza. Nitajitahidi kulieleza kwa kifupi.
Wakati nilipokuwa katika ziara kule Songea juraa la pili la mwezi uliopita, ilitangazwa habari kutoka Uganda kwamba Jeshi la Tanzania limeingia Uganda, limechukua sehemu kubwa ya Uganda, na linaua watu ovyo.

Siku hiyo ulipotangazwa uwongo huo nilikuwa nimealikwa kwenye chakula na vijana wetu wa Jeshi la Wananchi pale Songea. Kwa hiyo nikachukua nafasi hiyo kukanusha uongo huo, na kwa kweli kuwalaumu hao waliozua uwongo, na pia kuvishutumu vile vyombo vya habari duniani ambavyo vinapenda sana kutangaza-tangaza uwongo wa Amin.