Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana; uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai! Bila ya kuku hupati mayai; na bila mayai kuku watakwisha. Vile vile, bila ya uhuru hupati maendeleo, na bila ya maendeleo ni dhahiri kwamba uhuru wako utapotea.
Uhuru unategemea maendeleo. Tunapozungumza habari za uhuru maana yetu nini hasa, Kwanza, kuna uhuru wa nchi; yaani uwezo wa wananchi wa Tanzania kujipangia maisha yao, wakijitawala wenyewe bila ya kuingiliwa kati na mtu ye yote asiyekuwa Mtanzania.
Pili, kuna uhuru wa kutosumbuliwa na njaa, maradhi, na umasikini. Na tatu, kuna uhuru wa mtu binafsi; yaani haki yake ya kuishi, akiheshimika sawa na wengine wote, uhuru wake wa kusema na uhuru wake wa kushiriki katika uamuzi wa mambo yote yanayogusa maisha yake, na uhuru wa kutokamatwa ovyo na kutiwa ndani kwa kuwa tu kamuudhi mkubwa, japo kama haku-vunja sheria yo yote. Yote hayo ni mambo yanayohusu uhuru, na hatuwezi kusema kuwa Wananchi wa Tanzania ni huru, mpaka tuwe tuna hakika kwamba wanao uhuru wa mambo yote hayo.